Viongozi wa Iran wameshuhudia maandamano kwa siku ya pili mfululizo baada ya kukiri kudungua ndege ya abiria ya Ukraine na kusababisha vifo vya watu wote 176 waliokuwemo ndani wengi wao wakiwa raia wa Iran.
Maandamano yanashuhudiwa kote Tehran na miji mengine huku wengi wao wakipaza dhidi ya uongozi.
Inasemekana kwamba kumetokea vurugu huku vikosi vya usalama na vitumia vitoza machozi kutawanya waandamanaji.
Iran ilikubali kudungua ndege hiyo baada ya kukanusha kufanya hivyo hapo awali, na kusababisha wasiwasi zaidi kati ya nchi hiyo na Marekani.
Ndege hiyo iliyokuwa ikielekea mji mkuu wa Kyiv, ilidunguliwa karibu na mji wa Tehran Jumatano iliyopita, muda mfupi baada ya Iran kurusha makombora dhidi ya kambi mbili za kijeshi za Marekani nchini Iraq.
Mashambulizi hayo yalikuwa ni hatua ya kujibu mauaji ya afisa mkuu wa Iran Komanda Qasem Soleimani aliyeuawa kwenye shambulizi la ndege inayojiendesha yenyewe mjini Baghdad Januari 3.
Makumi ya raia wa Iran na Canada pamoja na raia wa mataifa ya Ukraine, Uingereza, Afghanistan na Sweden waliokuwa kwenye ndege hiyo waliaga dunia.
Nini kilitokea katika maandamano yaliyotokea Jumapili?
Waandamanaji walifanya maandamano mapya licha ya kuwepo kwa vikosi vingi vya usalama.
Polisi wa kukabiliana na ghasia, walinzi wa mapinduzi walikuwa kwa pikipiki na maafisa wa usalama waliokuwa wamevaa nguo za raia walikuwa tayari kukabiliana na waandamanaji.
Miongoni mwa yaliyoshuhudiwa yalikuwa yanapinga propaganda za serikali, mfano video iliyokuwa inaonesha wanafunzi wakiwa makini wasikanyage bendera za Marekani na Israel zilizochorwa katika chuo kikuu cha Shahid Beheshti mjini Tehran.
Katika baadhi ya ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, waandamanaji wanasikika wakitoa matamshi yanayopinga seerikali ikiwemo: "Wanadanganya kwamba adui wetu ni Marekani, Adui wetu tuko naye hapa." Wengi wa walioandamana walikuwa wanawake.
Video katika mitandao ya kijamii inaonesha waandamanaji wakipiga makofi na kupuza sauti zao katika uwanja wa Azadi uliopo Tehran. Mwanahabari wa BBC wa Uajemi amesema vikosi vya usalama vilivyopo uwanja huo vimekuwa vikirusha vitoza machozi kutawa waandamanaji.
Baadhi ya vyombo vya habari vimesema kwamba karibia watu 1000 walikuwa wanaandamana katika maeneo mbalimbali ya mji.
Aidha inasemekana kwamba maandamano yametokea katika miji mingine.
Kwa wale watakaoamua kuendelea na maandamano, watakuwa wanafahamu vyena uwezekano wa kutokea kwa vurugu kwasababu siku za nyuma vikosi vya usalama vimekuwa vikikabiliana na makundi kama hayo, amesema Sebastian Usher, mhariri wa BBC Arab.
Jumamosi, wanafunzi walikuwa wamekusanyika nje ya vyuo vikuu viwili. Awali wanafunzi hao walikusanyika kama njia ya kutoa heshima zao kwa walioaga dunia lakini maandamano yakazuka baadaye jioni na kuripotiwa kuwa maafisa wa usalama walifyatua vitoza machozi kutawanya waandamanji.
Magazeti kadhaa ya Iran yameangazia waathirika wa ndege hiyo kwa kutumia vichwa vya habari kama "Aibu" na "ni kitendo kisichoweza kusamehewa".
Gazeti moja linalopendelea serikali pia limeungwa mkono baada ya kukiri makosa.
Pia kumekuwa na maandamano yanayopinga mauaji ya Soleimani, na kushtumu Marekani na Uingereza.
Jumapili, Rais Donald Trump alirejelelea kuionya Iran kwamba isijaribu kulenga maandamano yanayopinga serikali, na kusema kuwa, "Dunia inafuatilia. Muhimu zaidi, Marekani inafuatilia karibu kinachoendelea".