Hii ni ATM kama ya fedha zinazotumika na Benki mbalimbali, lakini hii si ya fedha bali ya taulo za kike ama pedi za akina dada.
ATM hii itafungwa vyooni kwenye shule, ofisini, kwenye masoko ama kwenye saluni za kike, na ili kuitambua mahali ilipo inatumia App maalum katika simu.
David Msemwa, ni mmoja kati ya wabunifu wanne wa Mashine hii kutoka chuo cha Mtakatifu Joseph cha jijini Dar es salaam.
'' Mwanafunzi ama mtumiaji yoyote ataweza kujua Chausiku ipo wapi kwa kutumia simu yake, kuna programu maalum inayoonyesha uelekeo wa ATM zote za chausiku zilizo karibu yako''.
Mashine hii inatumia sarafu au kadi maalum ambayo hujazwa fedha na kukabidhiwa mwanafunzi. Msemwa anasema mwanafunzi ata "atapitisha" kadi kwenye mashine na kukatwa shilingi 2,000 ama 2,500 kulingana na aina ya pedi iliyowekwa kwenye mashine, na kadi ikiisha fedha anaweza kutumia sarafu ya shilingi 500 na kuitumbukiza kwenye sehemu maalum ya mashine hii akaweza kupata pedi kwa mtindo wa dharula.
Wasichana wengi wanaonekana kuipokea vyema mashine hii, wakiiona kama mkombozi hasa kwa wanaoona aibu kununua mbele za watu na wenye kipato cha chini.
Mariam Musa: " Chausiku ni mashine nzuri inakupa uwezo wa kununua pedi moja moja, kwa hiyo kama huna uwezo wa kununua bunda zima, hii ni nzuri sana, halafu pia nimeiona ni rahisi sana haina mbwembwe nyingi na lugha ngumu kama ATM zingine hasa za fedha".
Msichana kwa ajina Milembe Peter anasema: "Kwa upande wangu nimeipenda mashine hii hasa wakati wa dharula na wale ambao wanaona aibu kwenda kununua dukani hasa maduka ambayo wauzaji ni wanaume".
Wabunifu wa Mashine hii wametumia miezi minne kuja na ubunifu huu, ingawa haujakamilika asilimia mia moja, hatua iliyofikia ni ya kuboresha kitaalam zaidi.
Mkuu wa Kitengo cha ubunifu kutoka Chuo cha Mtakatifu Joseph, Dk Lawrence Kerefu anasema, kwa sasa mashine hiyo na vitu vingine vilivyobuniwa na wanafunzi wa chuo hicho, wameviwekea mkakati wa kuviboresha zaidi kabla ya kuanza kutumika.
'' Wabunifu hawa tutawaletea watalaamu kutoka nje kwa ajili ya kuwafundisha zaidi ili kupata bidhaa ama mashine zilizo kwenye viwango vya kimataifa na bora zaidi''
Anasema chuo hicho kinachowalea wabunifu wa mashine hii, kimeanzisha kitengo maalumu kulea wabunifu wengine takribani 45 kati ya wabunifu zaidi ya 200 waliobuni vitu mbalimbali.
Kwa sasa mashine ya Chausiku haijaanza kutumika kashuleni ama mtaani, ikitarajiwa kutumika wakati wowote kuanzia mwakani baada ya kuboresha kulingana na mazingira huku wanufaika wa kwanza wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuoni.