Rais John Magufuli |
Rais John Magufuli amewahakikishia walimu wote nchini kuwa serikali ipo tayari kulipa madeni ya walimu, baada ya madeni hayo kuhakikiwa.
Alisema hayo mjini Dodoma jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT). Pamoja na kulipa madeni ya walimu, Rais Magufuli alisema serikali inawajali walimu na ipo tayari kuboresha maslahi yao na kuboresha mazingira ya kazi kulingana na uwezo wake.
Aliwataka Watanzania wakiwemo walimu, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili nchi iwe na fedha za kutosha kuongezea maslahi hayo. Hata hivyo, alitoa mwito kwa walimu kuangalia upya matumizi ya michango ya asilimia mbili ya mshahara, anayokatwa kila mwalimu kila mwezi kwa ajili ya kuendesha CWT.
Alibainisha kuwa fedha zinazokusanywa ni nyingi na zingeweza kutumika kuwasaidia walimu, badala ya kuwekezwa katika miradi ambayo haimsaidii Mwalimu. Alitoa mfano wa mradi wa Benki ya Walimu, ambao mpaka sasa haujaanza na kuweka wazi kuwa mradi huo una dosari nyingi kulingana na taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ndio msimamizi mkuu wa benki hapa nchini.
Aliwatoa shaka walimu wote juu ya mchakato wa kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii. Alifafanua kuwa michango yao ipo salama, na mafao yao watayapata kama kawaida.
Alisema kwamba serikali inatarajia kuunganisha mifuko yote, inayowahudumia watumishi wa umma na kuwa mfuko mmoja; na wafanyakazi wa sekta binafsi, wataunganishwa katika mfuko mmoja ili kuongeza tija.
Mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo sasa ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Pesheni wa Watumishi wa Umma (PSPF) na Mfuko wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali Kuu (GEPF).
Mifuko miwli inayotarajiwa kubakia baada ya marekebisho yatakayofanyika mwakani ni NSSF kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta binafsi na PSPF kwa ajili ya watumishi wa umma. Rais alitoa mewito kwa CWT kutojiingiza katika masuala ya kisiasa, badala yake ijikite kupigania maslahi na ustawi wa walimu na kusimamia wajibu wa walimu.
“Kuna wakati hiki chama cha walimu kiligeuzwa kama chama cha siasa, msikubali kwenda kwa mwelekeo huo, hiki ni chombo muhimu, ni lazima kiende katika mwelekeo mzuri wenye manufaa, na mimi nataka kuwahakikishia kuwa nawapenda sana walimu, mimi mwenyewe nilikuwa mwalimu, nafahamu kila kitu kuhusu Ualimu,” alisisitiza Rais Magufuli.
Alitaka pia CWT ijiepushe na vitendo vya rushwa katika uchaguzi. Alionya kuwa vyombo vya dola vipo macho, kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya wote wanaojihusisha na rushwa. Kuhusu uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, Rais Magufuli alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto hiyo.
Alionya kuwa walimu ambao wamekuwa wakikataa kuripoti katika vituo vya kazi wanavyopangiwa na serikali, itawafuta kazi. Wakati huo huo, Rais Magufuli aliendesha harambee ya kuchangisha fedha na kufanikiwa kukusanya Sh milioni 60 za papo kwa papo, ambazo wajumbe wa mkutano huo pamoja na wanafunzi walioalikwa, watagawiwa