Kama hujawahi kuja Dar,basi unapolisikia jiji hilo picha pekee inayokujia kichwani mwako kwa mara ya kwanza ni majumba marefu, msongamano mkubwa wa watu na maeneo yenye pilika pilika za kila namna.
Waswahili husema penye wengi pana mengi na ndivyo ambavyo jiji hili linasadifu msemo huu, ambapo uwepo wa watu wengi wasiokuwa na ajira na hivyo kila uchwao hutafuta mbinu za kupata fedha kupitia wengine.
Leo nataka kukujuza mbinu tano wanazotumia wezi kupata fedha na kupora vitu mbalimbali kwa watu, maana mjini shule lakini wanaokuja hawaji na daftari hivyo ujanja wa kuwabaini matapeli na wezi ndio unaotakiwa.
1.MAZINGAOMBWE
Mbinu hii hutumiwa katika namna tofauti, mwizi humfuata anayetaka kumuibia au kumtapeli huku akiwa na dawa za kupumbaza akili.
Akishakutia dawa kwa namna wanazojua wenyewe, atakutaka umpe chochote na baadae unajikuta peke yako na tayari ushaingizwa mjini.
Kwa upande mwingine pia hutokea kama vile anauza simu barabarani. Atakuonesha simu kukutajia bei ndogo sana isiyofanana na bidhaa yenyewe.Ukiingia mfukoni tu, anakubadilishia na kukupatia simu mbovu au sabuni badala ya simu.
2.VISHANDU
Hapa wezi hutumia pikipiki ama gari na kuwapora watembea kwa miguu mikoba, simu na vingine vingi. Mara nyingi wezi hutokea kwenye barabara ambazo hazina pilika pilika yingi.
Lakini pia wezi hawa huwapora abiria katika daladala au magari, wakati wa foleni, unakuta abiria amejisahau na simu yake mara ghafla dirishani wanaipora.
Ukikaa siti ya dirishani, kuwa macho sana pindi unapotumia simu yako ndani ya basi au gari binafsi.
3.MCHEZO WA KARATA
Mchezo huu maarufu hufahamika kama ‘chafu tatu’ ni mchezo ambapo huwa na utapeli mkubwa, mtu hujikuta katoa pesa au simu na hawezi kuvipata tena bila ya kujijua.
Hapa huwa na kikundi cha watu waliojikusanya wakicheza mchezo huo wote wakiwa matapeli. Mgeni anapopita hukaribishwa kwa kupewa fedha mkononi na kucheza, baadae kumtaka atoe simu au fedha ili apate zaidi na hapo ndipo hutapeliwa na kukosa msaada wowote.
4.WIZI KUPITIA KWENYE MADIRISHA
Wizi huu maarufu hujulikana kama ‘jordan’ na hutokea mara nyingi katika nyumba za kupanga ama vyumba vya kulala wageni uswahilini.
Wezi huchana tundu dirishani na kuiba simu na vitu vingine kwa kutumia fimbo iliyotengenezewa kikapu ‘jordan” wakati wewe umelala.
5.NJIA YA SIMU
Hapa mwizi humpigia simu mtu anayehitaji kumtapeli na kujitambulisha kwa jina huku akidai kuwa wanafahamiana.
Wizi huu ni level nyingine kabisa maana atazungumza na wewe biashara na anaweza kukutumia hela mara kadhaa ili umwamini.
Siku atajifanya ana shida ghafla na kukuomba umtumie kiasi kikubwa tofauti na alizokutumia wewe, ukituma tu umeumia… ndio mwisho wa mawasiliano.
kuna mbinu nyingi sana ,hizo hapo juu ni baadhi tu ,kikubwa nikuwa makini hasa unapokutana na mtu ambae humfahamu alafu ukakuta anakusemesha.
Post a Comment
0Comments
3/related/default