Pengine tayari unafahamu kuwa kutokujishughulisha na mazoezi ya viungo mara kwa mara ni hatari kwa afya yako. Ndiyo hilo ni jambo ambalo kila mtu analijuwa (common sense).
Vipi lakini ikiwa ni kweli unajitahidi kila siku kutimiza jukumu hilo la kufanya mazoezi dakika 30 hadi lisaa limoja na wakati huo huo unatumia masaa mengi ukiwa umekaa kwenye kiti, ukiangalia TV masaa mengi, masaa mengi umekaa na una kazi katika Kompyuta?.
Ndiyo wewe unadhani kwakuwa unaenda kufanya mazoezi kila siku basi hiyo inatosha, si ndiyo?.
Ukweli ni kuwa hata kama wewe ni mtu wa kutembeatembea hapa na hapa lakini kama masaa mengine mengi yanatumika ukiwa umekaa kwenye kiti, mwili wako unakuwa karibu na magonjwa mengi bila mwenyewe kutambua.
Haya ndiyo madhara 7 ya kiafya utakayoyapata ukiwa ni mtu wa kupenda kukaa masaa mengi kwenye kiti au chini kila siku:
Kukaa muda mrefu kwenye kiti husababisha kufa mapema
1. Kunakosesha kupata oksijeni ya kutosha
Mara nyingi ukiwa umekaa unapenda kuegemea mgongo na siyo kukaa wima umenyooka, matokeo ya mkao huu ni kuzuia oksijeni kutembea kwa uhuru wote ndani ya mwili na mapafuni kwa ujumla.
Kisayansi tunapumua kwa uhuru wote tukiwa tumesimama na siyo tukiwa tumekaa.
Ukiwa umesimamaa ndipo mapafu hupata uwezo wa kujitanua mpaka mwisho na hivyo kuweza kutoa hewa chafu na kuingiza hewa safi ndani kiurahisi zaidi. Hali hii ya kukosa oksijeni ya kutosha mwilini hujulikana kwa kitaalamu kama ‘hypoxia’.
Wanasema kukaa kwenye kiti masaa matatu tu ni sawa na mtu aliyevuta sigara 6. Bila kupata oksijeni ya kutosha mwilini mwako kunapelekea magonjwa mengi mwilini bila idadi.
2. Unapata kirahisi kansa ya titi na kansa ya tumbo
Kansa ya titi na kansa ya utumbo mpana mara nyingi imeonekana kujitokeza kwa watu wa kula kulala yaani wale wasiopenda kujishughulisha na mazoezi ya viungo.
Kituo cha kudhibiti magonjwa cha Marekani (CDC) kimesema maisha ya kula kulala yanaweza kukuweka kuwa karibu karibu na kansa kwa zaidi ya 40%.
Hii ndiyo sababu wanawake wengi wanapatwa na kansa ya matiti miaka hivi karibuni sababu wengi wao ni watu wa kukaa tu nyumbani masaa mengi tofauti na wanaume ambao hutembea huku na huko kutafuta riziki ya kila siku.
Kuepuka kansa ya matiti na kansa ya utumbo mpana epuka kukaa kwenye kiti masaa mengi.
3. Una uwezekano mara 147 zaidi wa kupatwa na maradhi ya moyo
Matatizo katika mfumo wa upumuwaji ndiyo moja ya matokeo makubwa unaweza kuyapata ukiwa ni mtu wa kupenda kukaa kwenye kiti masaa mengi.
Ni matokeo ya kutokupata oksijeni ya kutosha kama matokeo ya kukaa kwenye kiti masaa mengi. Kwenye utafiti mmoja uliohusisha watu 800,000, wale waliokuwa wakikaa kwenye kiti masaa 10 kila siku walikuwa na uwezekano mara 147 zaidi wa kupatwa na magonjwa ya moyo kuliko wale waliokaa kwenye kiti masaa machache au mara moja moja.
Kuna tafiti nyingi zinazokubaliana na nadharia hii na inatokana na ukweli kwamba ukiwa umekaa ni rahisi mafuta mengi kujilundika mwilini mwako kuliko ukiwa umesimama.
Kadri unavyokaa masaa mengi kwenye kiti ndivyo vimeng’enya vinavyofanya kazi ya kuchoma mafuta mwilini vinavyokuwa na nguvu chache kuchoma hayo mafuta. Na tatizo la unene au uzito kupita kiasi lina uhusiano wa moja kwa moja na matatizo mbalimbali ya moyo.
4. Itakuwa vigumu kitambi na uzito kukuisha

Madhara ya kukaa muda mrefu kwenye kiti
Umewahi kujaribu kufanya mazoezi, kubadili chakula au hata kufunga na bado ukawa unasumbuliwa na kitambi au uzito kuwa mkubwa? Basi jibu la tatizo lako ni kukaa kwenye kiti masaa mengi.
Utafiti unaonyesha kukaa tu kwenye kiti hata kama hauli chakula kingi bado utaendelea kuongezeka uzito.
Kwahiyo kama unataka kuondoa kitambi au tumbo au kupungua uzito kwa haraka acha kukaa masaa mengi kwenye kiti, hata kama kazi yako ni ya ofisini jaribu namna unaweza kupata meza ya kusimama huku unaendelea na kazi yako.
5. Ni rahisi kupatwa na ugonjwa wa Kisukari
Unataka kupona au kuepukana na Kisukari aina ya pili? Basi acha kukaa kwenye kiti muda mrefu.
Moja ya hatari zaidi za kukaa kwenye kiti masaa mengi ni kuwa mwili unakuwa hauitiki vema kwa insulin jambo ambalo ni matokeo ya kukaa masaa mengi kwenye kiti na hii ni matokeo ya kuzalishwa kwa wingi kwa kongosho kupita inavyohitajika kama matokeo ya kukaa muda mrefu.
Wakati ukiwa umekaa tu kwenye kiti kongosho linaendelea kutengeneza insulin lakini katika mwili huo uliokaa tu, insulin inakuwa haitumiki vema na mwili jambo linalomaanisha kuwa damu sukari (glucose) haiondolewi kwenye mzunguko wa damu kwa haraka.
Hivyo uwezekano wa kupata Kisukari unaongezeka kwa zaidi ya asilimia 14 kwa Yule mwenye tabia ya kukaa masaa mengi kwenye kiti kuliko mtu mwingine yoyote.
6. Utapatwa na maumivu ya nyuma ya mgongo
Ukiwa ni mtu wa kupenda kukaa kwenye kiti masaa mengi kuna uwezekano ukawa haukai hata mkao mzuri kiasi cha kuwa karibu na maumivu ya mgongo kila mara. Watu wa namna hii pia huwa na maumivu ya kwenye uti wa mgongo kila mara.
Kwa mjibu wa utafiti wa Taasisi ya ‘DNA India’ wagonjwa wengi wenye matatizo ya uti wa mgongo ni wale wenye miaka 20 na 30 na wengi wao ni wale hufanya kazi wakiwa wamekaa kwenye kiti masaa mengi.
Miaka ya sasa ni rahisi kukutana na watu wanaolalamika kupatwa na maumivu ya mgongo na wengi wao ukiwachunguza ni wale wanaotumia masaa mengi kukaa kwenye kiti.

madhara ya kukaa muda mrefu kwenye kiti
7. Utakufa ukiwa bado kijana
Shirika la afya duniani limesema mtindo wa kukaa masaa mengi kwenye kiti ndiyo unaohusika na kuongezeka kwa uzito na unene kupita kiasi katika nchi nyingi zilizoendelea.
Na uzito kupita kiasi ni moja ya tatizo kubwa la afya kwa mtu mzima yoyote kuwa nalo ingawa wengi hawaelewi hilo, wengi hasa waAfrika wakiwa wanene au wenye uzito mkubwa ndiyo hudhani hiyo ni afya.
Uzito na unene kupita kiasi huja na matatizo mengine makubwa ikiwa ni pamoja na matatizo katika mfumo wa upumuwaji, kisukari, stroke, kukosa usingizi nk na haya yote yanaweza kupelekea wewe kufa ukiwa bado kijana.
Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Harvard mwaka 2014 ulitoa hitimisho kwamba kukaa kwenye kiti masaa mengi ni moja ya sababu ya vifo vya mapema kwa watu wengi.
Mtandao wa Huffington ulienda mbali zaidi na kusema kukaa kwenye kiti masaa matatu tu kwa siku ni sawa na mtu aliyevuta sigara 6 na kuwa kukaa kwenye kiti masaa mengi kunaua watu wengi zaidi duniani kote kuliko hata UKIMWI.
Mara ya kwanza niliposoma habari hizi nilishikwa na mshangao wa ajabu maana mimi mwenyewe nimekuwa mtu wa kukaa kwenye kiti kwa miaka mingi sasa kwani kazi zangu nyingi huzifanya nikiwa kwenye computer.
Yaani haikuchukuwa muda nikabadili mkao tayari ninafanya kazi zangu nikiwa nimesimama, na tayari nimeona mabadiliko makubwa kwenye afya yangu kwa ujumla.
Pamoja na kuwa kusimama ni bora zaidi kuliko kukaa, bado unatakiwa utumie muda fulani kukaa pia, usisimame masaa yote kutwa nzima, ukisimama masaa matatu tumia nusu saa nyingine kukaa hivyo hivyo mpaka siku yako inaisha.
Nini maoni yako? umekaa muda mrefu kwenye kiti na unapata mojawapo ya madhara yaliyoandikwa hapa? nipe uzoefu wako.
Post a Comment
0Comments
3/related/default