ZITTO KABWE AOMBA MSAADA UKAWA



Mwaka 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu ilishuhudiwa Chama cha ACT- Wazalendo kikijiweka kando na vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vilivyoungana kuiondoa CCM madarakani kwa kuachiana majimbo na kata.

ACT-Wazalendo ilisimamisha mgombea urais, wabunge na madiwani katika uchaguzi huo uliokuwa wa vuta - nikuvute waliochuana na CCM pamoja na wa Ukawa unaoundwa na Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi.

Ikiwa ni miaka mwili imepita tangu kufanyika kwa uchaguzi huo, kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe ameibuka na kuomba ushirikiano kwa vyama vya upinzani hasa vya Ukawa katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata mbili kati ya tatu za Mkoa wa Dar es Salaam.

Uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 26 nchi nzima utashirikisha kata 43, huku Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma mjini tayari ombi lake hilo kwa Ukawa limepata vikwazo akitakiwa kuliwasilisha kwa njia ya maandishi.

Wakati vyama hivyo vikimtaka kutumia utaratibu huo kuwasilisha ombi lake ili kuona uwezekano wa kumuachia kata hizo, yeye amesema ni wakati wa kuweka kando tofauti za kihistoria na waungane kupambana na adui yao, CCM.

Juzi, Zitto alizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kata anazoomba kuachiwa ni ya Saranga na Kijichi, huku ile ya Mbweni akiwa hajasimamisha mgombea. Ombi hilo linaweza kuwa njia ya ACT - Wazalendo kutaka kujiunga na Ukawa.

Akizungumzia ombi la Zitto, mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema, “Zitto anajua utaratibu. Afuate utaratibu wa kuwasiliana na viongozi wenzake si kwa kutumia vyombo vya habari, kwa kuwa suala hilo ni zito na linahitaji majadiliano.”

Alipoulizwa akitumia utaratibu huo watakuwa tayari kumwachia kata hizo, Mrema alisema, “Tuna vikao tutakaa, kujadili na kushauriana. Suala la utayari utategemea hoja ambazo yeye atazisema na kuwashawishi wenzake kwa nini tumwachie, hivyo kama nilivyosema atumie utaratibu tu kuwasilisha maombi yake.”

Ingawa Chadema wametoa kauli hiyo, kunaweza kukawa na ugumu wa kuyapokea maombi hayo na kuyafanyia kazi kutokana na mgawanyiko uliopo ndani ya CUF.

Chama cha Wananchi CUF kimegawanyika pande mbili; ile inayomuunga mkono katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na nyingine ya mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Upande wa Maalim Seif unaamini kuwa ndani ya Ukawa, lakini Profesa Lipumba amekuwa akiupinga kwamba hauna tija.

Kwa maana hiyo, ombi la Zitto litakuwa na wakati mgumu kushughulikiwa kutokana na Ukawa ya mwaka 2015 kuwa tofauti na ya sasa ambayo katika kipindi cha hivi karibuni haijawahi kuonekana ikifanya vikao.

Katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Ukawa walikuwa wakiachiana kata na majimbo kwa kusimamisha mgombea mmoja hivyo kupata wabunge na madiwani wengi, huku ACT - Wazalendo ikishinda jimbo la Kigoma Mjini aliloshinda Zitto ilhali mgombea wake wa urais, Anna Mghwira akipata kura 98,763 (sawa na asilimia 0.65).

Muungano huo wa Ukawa licha ya kushindwa na mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kwa kupata kura 8,882,935 (sawa na asilimia 58.46), mgombea wao wa urais, Edward Lowassa alipata kura 6,072,848 (sawa na asilimia 39.97) zikiwa ni nyingi kuliko walizowahi kupata wapinzani kwa nafasi hiyo tangu kuanza kwa uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi mwaka 1995.

Zitto alipotafutwa na SWAHIBA BLOG  ili kujua iwapo amewasilisha maombi kwa maandishi, alisema hajafanya hivyo.

Hata hivyo, mgombea wa ACT- Wazalendo, Merycer Matale imeelezwa hajateuliwa katika taarifa ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Saranga, Dandasi Kijo. Waliopitishwa ni Haroun Mdoe wa CCM na Abeid Rutozi wa CUF. “Kampeni zimeanza. Hatuna muda wa urasimu. Kuna kata tatu, tunapaswa kushinda Dar es Salaam. Dar es Salaam ndiyo kitovu cha siasa nchini, kuingiza urasimu ni kupoteza muda,” alisema Zitto.

“Sisi tumeanza kampeni leo (jana) Kijichi. Tunawatakia kila la heri Mbweni wenzetu wa Chadema. Wito wangu tuweke tofauti za historia pembeni na tukampige adui.”

Katika uzinduzi wa kampeni jana, alisema wakichaguliwa wataondoa ugumu wa maisha na ukiukwaji wa haki.

Akizungumzia ombi la Zitto, kaimu naibu mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa CUF upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande alisema, “Suala hilo na mengine hadi tujadili na kesho (leo) tutatoa taarifa hili lazima lijadiliwe na je, tutakuwa tumelipokea kama taarifa rasmi.”

Kwa upande wake, naibu mkurugenzi wa Habari - CUF, upande wa Profesa Lipumba, Abdul Kambaya alisema hawawezi kuachiana maeneo ya uchaguzi kama nyanya sokoni.

“Zitto anapaswa kujua kwamba mwenye kura chache anamuunga mwenye kura nyingi,” alisema.

Kambaya alisema katika uchaguzi huo wamesimamisha wagombea 34 na jana alianza kampeni katika Kata ya Saranga.

Chadema wakata rufaa

Katika hatua nyingine, taarifa iliyotolewa jana na mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene ilieleza wamekata rufaa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya wagombea wao sita kuenguliwa.

Wagombea hao, kata na mikoa kwenye mabano ni Kinyafu Alphonce, (Saranga-Dar es Salaam), Gerald Justine (Siuyu-Singida), Onesmo Kambona (Mnacho, Lindi), Emmanuel Salewa (Ngabobo, Arusha), Joyce Ruto (Makiba, Arusha) na Michael Kayange (Kalambo, Songwe).

Makene alisema utaratibu na masharti ya kumuwekea mgombea pingamizi haukufuatwa na kwamba, baadhi yao wamewekewa pingamizi kuwa si wakazi wa kata husika jambo ambalo siyo la kweli kwa kuwa Saranga na Siuyu wagombea hao walishawahi kugombea awali.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima alipotafutwa kwa simu ya kiganjani alimtaka mwandishi kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi (sms) ambao hata hivyo hakuujibu.



Post a Comment

Previous Post Next Post