Mwanamkakati wa Maalim Seif Aswekwa Ndani Na Jeshi La Polisi Zanzibar

Unknown
By -
0
Mwanamkakati  wa aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Mohamed Sultan Mugheiry, maarufu kwa jina la Eddy Riyami, amewekwa ndani na Jeshi la Polisi mjini Unguja kwa tuhuma za kumtukana Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Eddy Riyami ambaye ni mmoja wa wana mkakati wa timu ya ushindi wa aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikutwa na mkasa huo jana baada ya kuitwa polisi kutoa maelezo kutokana na tuhuma zinazomkabili.

Riyami ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, alikwenda Polisi Makao Makuu kuitikia wito wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, SSP Simon Pasua, huku akiandamana na Mwanasheria wa CUF, Masoud Faki Masoud.

Mwanasheria huyo jana alisema Riyami anatuhumiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya kimtandao.

Alisema licha ya kuzikana tuhuma hizo, lakini Jeshi la Polisi bado lilimshikilia kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Ni kweli ameshikiliwa na polisi kwa ajili ya kupitisha uchunguzi na yupo Polisi Madema, eti Eddy kaambiwa kamtukana Dr. Shein kwenye ‘audio’ ambayo hata si sauti yake, lakini dhamana ipo wazi na tutamchukulia dhamana,” alisema Masoud.

Akizungumzia kukamatwa kwa Riyami, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Salum Msangi, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Kitu ninachoweza kuthibitisha ni kuwa tunamshikilia Riyami kwa ajili ya kupitisha uchunguzi,” alisema Naibu Kamishna Msangi.
 
Februari 15, mwaka huu Ofisi ya Mkurunzi na Makosa ya Jinai, ilimwandikia Riyami barua ya wito na kumtaka kufika ofisi ya upelelezi iliyopo Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.

Riyami alitii wito huo ambapo wiki iliyopita alikwenda lakini mmoja wa maofisa wa Jeshi la Polisi aliyemwandikia barua alikuwa nje ya Zanzibar kwa shughuli za kikazi na kumtaka kwenda jana jumatatu

Riyami si mwanachama wa CUF, lakini mara kadhaa amekuwa akitumiwa na chama hicho kwa ajili ya mikakati mbalimbali pamoja na ushauri.
Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)