Timu 3 za kijeshi kati ya nne zimehusika katika ‘tuhuma’ za upangaji wa matokeo ili kumpata mshindi atakayepanda ligi kuu msimu ujao kutoka kundi la 3 la ligi daraja la kwanza iliyomalizika wikendi-jana.
Ruvu Shooting ya Pwani ilikuwa timu ya kwanza kupanda VPL msimu ujao kutoka kundi la B, ubora wao uliwafanya wapande wakiwa na michezo mitatu mkononi. Hakika wamestahili pongezi kwa jitihada kubwa walizofanya mara baada ya kushuka msimu uliopita.
African Lyon pia imerejea ligi kuu baada ya kukamilika kwa mechi za kundi A siku ya Jumapili. Lakini timu ya tatu haijatangazwa na Shirikisho la mpira nchini, TFF lakini kwa asilimia mia moja itapaswa kuwa Mbao FC ya Mwanza ambayo hadi siku ya mwisho ya michezo ya kundi A ilikuwa katika nafasi ya nne.
Kwanini, Mbao FC wanapaswa kupanda kutoka kundi C badala ya timu za Geita Gold Sports, Polisi Tabora na JKT Oljoro ambazo zilimaliza katika nafasi 3 za juu katika kundi.
Katika ligi ambayo hakuna timu iliyowahi kushinda zaidi ya magoli 5-0 katika kundi si rahisi zipatikane ‘mechi mbili double’ zenye idadi kubwa ya magoli. Geita imeishinda 8-0 JKT Kanembwa ya Kigoma katika uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma siku ya Jumamosi.
Inawezekana kabisa Geita walikuwa na uwezo wa kupanda kutokana na mwenendo wao wa msimu mzima kuwa wenye matokeo mazuri, ila njia ya mwisho waliyoitumia kutaka kupanda VPL ni mbaya na huenda ikawapoteza kabisa katika ramani ya mpira ikiwa tu itagundulika walipanga matokeo kwa namna yo yote ile.
Siku hiyo hiyo katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora wenyeji Polisi Tabora wakaichapa 7-0 JKT Oljoro ya Arusha. Oljoro ile iliyopiga mpira mwingi siku chache nyuma dhidi ya Geita Gold Sport isingeweza kufungwa 7-0 tena magoli 6 wakiruhusu katika dakika 45 za kipindi cha pili.
Katika baadhi ya vyombo vya habari baadhi ya mashuhuda walisema kulikuwa na asilimia nyingi kuashilia ulikuwapo upangaji wa matokeo huku jina la Jamal Malinzi (rais wa TFF) likihusika kama mtu aliyekuwa akitoa maelekezo ya nini kinapaswa kufanyika katika uwanja wa Lake Tanganyika.
Hizi ni tuhuma za wazi amekuwa akitupiwa Malinzi kuhusu michezo hiyo ‘tata’ zinaweza kumfanya kuchukua maumuzi magumu ya kufuta matokeo ya timu hizo nne (Geita, Kanembwa, Polisi Tabora na Oljoro) kuzishusha daraja na kuwafungia wale wote ambao walihusika ikiwa itabainika matokeo yalipangwa.
Kushindwa kulisimamia hili na kulitolea maamuzi sahihi itamaanisha ameshindwa, na kama atashindwa katika hili atapaswa tu kujiuzulu. Hakuna sababu ya kuchezwa kwa ‘playoff’ kati ya Geita na Polisi kwa kuwa timu zote zimefungana kwa kila kitu.
Kama mechi zao zingemalizika wa matokeo yaliyokuwapo kipindi cha kwanza ( Polisi Tabora 1-0 JKT Oljoro, JKT Kanembwa 0-1 Geita Gold Sport) bila shaka sasa tungezifahamu timu zote 3 zilizopanda lakini kwa kile kilichojitokeza katika dakika 45 za mwisho, yakiwemo matukio ya mechi kusimama kwa muda mrefu bila sababu za msingi ni dalili ya za wazi kuwa matokeo yalipangwa.
Ikiwa matokeo ya timu hizo yatafutwa kama inavyotarajiwa na kushushwa daraja, timu ya Mbao FC itakuwa na nafasi ya kuongoza kundi na hivyo watacheza VPL msimu ujao. Malinzi hii ni nafasi yake ya kujimaliza kiuongozi au kufufua upya mtazamo wake alioingia nao madarakani miaka miwili iliyopita.
Kushindwa kuzishusha daraja na kuzifungia timu hizi atakuwa ameshindwa, maamuzi sahihi yatamsafisha na kumuweka katika viongozi wa mfano.
Chanzo : Shaffih Dauda
Chanzo : Shaffih Dauda