Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Licha ya kusisitiza kuwa straika wake, Pape Ndaw ni mshambuliaji makini na mwenye uwezo mkubwa mkufunzi mkuu wa Simba SC, Dylan Kerr atalazimika ‘kum-bust’ mshambuliaji na nahodha wa timu hiyo Musa Hassan Mgosi ili kukabiliana na tatizo la washambuliaji katika timu yake.
Simba ipo Mbeya tangu Jumatatu hii kwa ajili ya gemu mbili dhidi ya Mbeya City FC siku ya Jumamosi na Tanzania Prisons siku ya Jumatano ijayo katika uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mganda na kinara wa ufungaji wa timu hiyo Hamis Kiiza anasumbuliwa na majeraha, Daniel Lyanga itabidi aendelee kusubiri hadi wakati wa usajili wa dirisha dogo na ili kukabiliana na City, Kerr atalazimika kumtegemea zaidi Mgosi sambamba na chipukizi, Ibrahim Ajib, Boniface Maganga na Msenegal, Ndaw.
“Ndaw ni mshambuliaji mwenye vigezo, ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga pasi na kufunga”, alikaririwa Kerr akimsifia mshambulizi huyo mrefu zaidi katika ligi kuu Tanzania bara msimu huu.
Kiiza ametupia kambani magoli matano kati ya 7 ya Simba katika gemu tano zilizopita, aliukosa mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar ambao Kerr alimpanga kiungo mchezeshaji Peter Mwalyanzi katika idara ya mashambulizi sambamba na Ajib.
Faraja kubwa kwa Simba ni kurejea katika kiwango kwa kiungo wao Jonas Mkude. Mechi hiyo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa kandanda nchini ambao wanataka kuona ni vipi City itaanza maisha mapya bila mwalimu Juma Mwambusi aliyejiunga na Yanga. Simba haijawahi kupata ushindi katika gemu nne zilizopita dhidi ya City na mara ya mwisho walipokutana ‘Wekundu wa Msimbazi’ walilazwa 2-0.
Simba imeshinda gemu nne, imepoteza mechi moja na ipo nafasi ya 3 ya msimamo ikiwa na alama 12 sawa na Mtibwa Sugar lakini kikosi cha Kerr kina wastani mzuri wa magoli ya kufunga na kufungwa kuliko Mtibwa. Simba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu na kufanya wawe na wastani wa magoli Manne ya kufunga na kufungwa.
Tags
Michezo
